Psalms 44

Kuomba Ulinzi Wa Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Utenzi Wa Wana Wa Kora)


1 aEe Mungu, tumesikia kwa masikio yetu,
baba zetu wametueleza
yale uliyotenda katika siku zao,
siku za kale.

2 bKwa mkono wako uliwafukuza mataifa
na ukawapanda baba zetu,
uliangamiza mataifa
na kuwastawisha baba zetu.

3 cSio kwa upanga wao waliipata nchi,
wala si mkono wao uliwapatia ushindi;
ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume,
na nuru ya uso wako,
kwa kuwa uliwapenda.


4 dWewe ni mfalme wangu na Mungu wangu,
unayeamuru ushindi kwa Yakobo.

5 eKwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu;
kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.

6 fSiutumaini upinde wangu,
upanga wangu hauniletei ushindi;

7 gbali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,
unawaaibisha watesi wetu.

8 hKatika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa,
nasi tutalisifu jina lako milele.


9 iLakini sasa umetukataa na kutudhili,
wala huendi tena na jeshi letu.

10 jUmetufanya turudi nyuma mbele ya adui,
nao watesi wetu wametuteka nyara.

11 kUmetuacha tutafunwe kama kondoo
na umetutawanya katika mataifa.

12 lUmewauza watu wako kwa fedha kidogo,
wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao.


13 mUmetufanya lawama kwa jirani zetu,
dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka.

14 nUmetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa,
mataifa hutikisa vichwa vyao.

15 oFedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa,
na uso wangu umejaa aibu tele,

16 pkwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana,
kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi.


17 qHayo yote yametutokea,
ingawa tulikuwa hatujakusahau
wala hatujaenda kinyume na agano lako.

18 rMioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma;
nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako.

19 sLakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha,
na ukatufunika kwa giza nene.


20 tKama tungalikuwa tumelisahau jina la Mungu wetu
au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni,

21 uje, Mungu hangaligundua hili,
kwa kuwa anazijua siri za moyo?

22 vHata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;
tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.


23 wAmka, Ee Bwana! Kwa nini unalala?
Zinduka! Usitukatae milele.

24 xKwa nini unauficha uso wako
na kusahau taabu na mateso yetu?


25 yTumeshushwa hadi mavumbini,
miili yetu imegandamana na ardhi.

26 zInuka na utusaidie,
utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.
Copyright information for SwhKC